Thursday, November 10, 2016

Azam wamuenzi vyema Mzee Said Mohamed, yatoa kipigo kitakatifu kwa Mwadui


AZAM FC leo wamemuenzi vyema Mzee Said Mohamed kwa kuishushia kipigo cha mbwa mwizi Mwadui FC cha mabao 4-1, mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Mwadui mkoani Shinyanga.
Katika mchezo huo ambao timu zote mbili zilianza kwa hofu kubwa kutokana na kutokuwa na matokeo mazuri katika michezo yao iliyopita, Mwadui walipata goli dakika ya 20 kupitia kwa Jerryson Tegete lakini mwamuzi alikataa kwa madai kwamba aliunawa kabla ya kufunga.
Haikuishia hapo, Hassan Kabunda akaweka goli safi kwa bicycle kick dakika ya 30 na kuwapa Azam FC wakati mgumu.
Dakika ya 36 Azam FC walifanya mabadiliko baada ya Mudathir Yahya kutoka kufuatia kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Ramadhan Singano.
Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Mwadui kutoka kifua mbele katika uwanja wao wa nyumbani.
Azam walifanya tena mabadiliko kwa kumtoa Gadiel Michael na nafasi yake kuchukuliwa na Shaaban Idd mnamo dakika ya 53 na baadaye mabadiliko mengine kufanywa kwa kutoka Frank Domayo na kuingia Francisco Zekumbawira.
Mabadiliko hayo yalionekana kuwa na mtazamo chanya baada ya Azam FC kufanikiwa kusawazisha bao kupitia kwa John Bocco dakika ya 54 kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Mwadui.
Shaaban Idd aliyeingia kutoka benchi aliipatia Azam bao la pili dakika ya 71, huku Mzimbabwe Zekumbawira ambaye pia aliingia kutokea benchi akifunga bao la tatu dakika ya 74.
Shaaban Idd kwa mara nyingine tena aliipa Azam bao la nne dakika ya 77 na kuvunja matumaini yote ya Mwadui ya kushinda mchezo huo uliofanyika katika dimba lao la nyumbani.
Matokeo yanaifanya Azam FC kumaliza mzunguko wa kwanza wa ligi ikiwa kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ikijikusanyia pointi 25 ikizidiwa 10 tu na vinara Simba waliojikusanyia 35, ambao jioni ya leo wamepoteza mchezo kwa kufungwa na Tanzania Prisons mabao 2-1, huku Mwadui wakiwa kwenye nafasi ya 14 na alama zao 13.

0 comments:

Post a Comment